Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

20 NOVEMBA 2026
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda UNIDO limechukua hatua kuendeleza viwanda hadi kusaidia wakulima wa migomba kutotupa mashina ya zao hilo badala yake kutengeneza hata taulo za kike.
Kwa hayo na mengine mengi, Assumpta Massoi wa Idhaa akiwa Nairobi, Kenya amezungumza na Naibu Mwakilishi wa UNIDO nchini humo Linet Luvai anayeanza kwa kuelezea umuhimu wa maendeleo ya viwanda. Karibu Linet.
Pia tunakuletea muhtasari wa habari.
• Leo ni siku ya siku ya Maendeleo ya Viwanda barani Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika ujumbe wake wa siku hii ametoa wito wa kuimarishwa kwa uwekezaji na ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi ili kuharakisha maendeleo ya viwanda barani Afrika. Guterres amehimiza kuongezwa nguvu kwenye sekta zinazokuwa kwa kasi kama vile magari yanayotumia umeme, utengenezaji wa betri, vipuri vya kompyuta na nishati jadidifu, na kueleza hizi zinafungua fursa mpya za kiuchumi kwa mataifa ya Afrika na kusaidia bara hilo kubadilisha uchumi wake, kuongeza ajira zenye tija, kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi na kujenga mustakabali wenye ustawi na uendelevu
• Leo pia ni Siku ya Kimataifa ya Watoto na shirika la Elimu Haiwezi Kusubiri, (ECW) limetangaza uwekezaji wa dola milioni 52 kusaidia zaidi ya watoto 300,000 kuendelea kupata elimu katika nchi za Lebanon, Myanmar na Sudan Kusini, ambazo zimeathiriwa na migogoro na majanga ya kibinadamu. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mkurugenzi wa ECW, Maysa Jalbout, amesema “Katika nchi zote tatu, angalau nusu ya watoto wanaofikiwa ni wasichana, na takriban mtoto mmoja kati ya kumi ana ulemavu. Hata hivyo, kufungua mlango wa darasa pekee hakutoshi kuwarejesha wasichana shuleni.”
• Na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limetangaza mpango wa kusaidia watu milioni 91 wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka 2027, na kwamba linahitaji zaidi ya dola bilioni 12 ili kutekeleza mpango huo.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Audio and video play straight from the show's own hosting. PodSubs stores and serves no media.

